Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu YDH, sambamba na kuongezeka kwa operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni katika maeneo yote ya Ukingo wa Magharibi, takriban Wapalestina wanane wamekamatwa wakati wa uvamizi wa vikosi vya uvamizi. Wakati huohuo, walowezi wa Kizayuni walivamia vijiji vya kusini mwa Nablus na kushambulia nyumba, magari na miundombinu ya umeme ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Shahab, vikosi vya uvamizi vilivamia maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi alfajiri ya Jumanne, vikafanya upekuzi katika nyumba za Wapalestina na kutumia risasi za moto, mabomu ya sauti na gesi ya kutoa machozi wakati wa operesheni hizo.
Mpalestina mmoja ajeruhiwa Nablus
Shirika la Mwezi Mwekundu la Palestina lilitangaza kuwa; wakati wa shambulio la vikosi vya uvamizi mashariki mwa Nablus, raia mmoja wa Kipalestina alijeruhiwa kwa kupigwa risasi za moto. Wanajeshi wa Kizayuni pia walirusha gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya wakazi wa eneo hilo.
Mashambulizi katika miji na kambi za wakimbizi za Ukingo wa Magharibi
Vikosi vya uvamizi pia vilivamia miji ya Qabatiya, Fahma na Kafr Rai katika mkoa wa Jenin, na katika operesheni zao huko Fahma na Kafr Rai vilitumia mabomu ya sauti.
Huko Tulkarm pia, wanajeshi wa Kizayuni walivamia miji ya Bala'a na Deir al-Ghusun, na kufanya upekuzi katika nyumba ya Muayyad Shaaban, Mkuu wa Kamati ya Kupambana na Ukuta wa Kutenganisha na Ujenzi wa Makazi ya Walowezi, ambapo nyumba hiyo iliharibiwa.
Kambi ya wakimbizi ya Al-Far'a, kusini mwa Tubas, pia ilizingirwa kwa saa kadhaa na vikosi vya uvamizi, huku nyumba nyingi katika kambi hiyo zikifanyiwa upekuzi.
Katika mji wa Azzun, ulioko katika mkoa wa Qalqilya, vijana sita wa Kipalestina walikamatwa, baadae vikosi vya uvamizi vilivamia vitongoji vya Kafr Saba na Zaid na kufanya upekuzi katika nyumba kadhaa.
Aidha, wafungwa wawili wa Kipalestina waliokuwa wameachiwa huru walikamatwa tena baada ya vikosi vya uvamizi kuvamia nyumba zao. Ripoti pia zinaeleza kuwa vikosi vya uvamizi vilivamia kambi ya Al-Fawwar na mji wa Tarqumiya katika eneo la Al-Khalil, pamoja na kutekeleza operesheni katika kitongoji cha Al-Masanaa mjini Ariha.
Mashambulizi ya walowezi kusini mwa Nablus
Sambamba na operesheni za jeshi la utawala wa Kizayuni, walowezi wa Kizayuni walivamia vijiji vya Talfit na Qalud kusini mwa Nablus. Washambuliaji walivamia nyumba za Wapalestina na kuchoma moto nyumba kadhaa pamoja na magari. Picha zilizochapishwa kutoka eneo la tukio zinaonesha magari ya Wapalestina yakiteketea kwa moto.
Bashar Al-Qaryuti, mmoja wa wanaharakati wa Kipalestina, alisema kuwa; walowezi walichoma moto magari matatu, walivamia nyumba za Wapalestina na pia waliharibu mtandao wa umeme wa eneo hilo.
Kuongezeka kwa mashambulizi tangu kuanza kwa vita vya Ghaza
Tangu kuanza kwa vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza mwezi Oktoba mwaka 2023, operesheni za kijeshi za utawala huo katika Ukingo wa Magharibi pamoja na mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni zimeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa takwimu za vyanzo vya Kipalestina, tangu wakati huo hadi sasa, takriban Wapalestina 1,179 wameuawa kishahidi katika Ukingo wa Magharibi, watu 12,666 wamejeruhiwa, na karibu watu 24,000 wamekamatwa.
Maoni yako